Chunusi matakoni

Chunusi Matakoni – Sababu na Tiba

Kuna watu wengi sana wanaosumbuliwa na tatizo sugu la chunusi matakoni.  Na ingawa chunusi zinaweza kutokea usoni, shingoni, kifuani, na mgongoni, chunusi za matako ni moja wapo wa chunusi sugu zaidi.

La kushangaza ni kuwa ugonjwa huu wa ngozi unaweza ukaathiri mtu mmoja na ukakosa kuathiri mwingine. Wanasayansi hawajaweza kujua kabisa sababu inayosababisha utafauti huu. Lakini utafiti unaonyesha kuwa chunusi hutokea wakati vitundu vya kutolea jasho ngozini vinapozibwa na bakteria, mafuta, au seli za ngozi zilizokufa.

Dalili za Chunusi Matakoni

Chunusi matakoni zinaweza kuwa zenye dalili nyepesi tu na kwa watu wengine dalili hizi zinaweza zikawa kali sana. Kwa kawaida, waathiriwa hupatwa na viuvimbe, madoa meupe, au madoa meusi kwenye makalio au sehemu ya mwili iliyoathirika.

Wakati mwingine mtu anaweza kupata vipele vidogovidogo ambavyo hata havionekani kwa urahisi. Viuvimbe hivi huwa havina uchungu na vinaweza vikaisha vyenyewe. Watu walio na chunusi kali hupatwa na athari mbaya na wakati mwingine, chunusi zile husababisha mwasho na maumivu hasaa zinaposuguliwa.

Sababu Kuu za Chunusi Matakoni

Chunusi zote huanza wakati vitundu vya kutolea jasho ngozi vinapozibwa. Vitundu hivi vinaweza kuzibwa na vitu mbalimbali kwa mfano:

·         Uzalishaji wa mafuta mengi sana kwenye ngozi

Katika sehemu ya chini ya ngozi zetu huwa kuna tezi zinazozalisha mafuta yanayofanya ngozi zetu laini na zinazopendeza. Lakini wakati mwingine, tezi hizi zinaweza kuzalisha mafuta mengi kupita kiasi. Mafuta haya huziba vishimo vya kutolea jasho na kusababisha chunusi. Hii ni mojawapo ya visababishi vikuu vya chunusi.

·         Homoni

Vijana wanapofikisha umri wa kubaleghe, kipimo cha homoni za ngono kinachotengenezwa mwilini huongezeka kwa kiasi kikubwa. Ongezeko hili husababisha chunusi matakoni, usoni, na kwenye sehemu zingine za mwili. Hali hii hutokea hasaa kwa watu walio kati ya umri wa 11 hadi 25.

Msuko huu wa homoni pia unaweza kutokea pale mwanamke anapoanza kutumia dawa za kupanga uzazi au anapofikisha umri wa kukoma kuzaa (menopause).

·         Seli za ngozi zilizokufa

Je wajua kuwa takriban seli elfu nne za ngozi zetu hufa kila dakika? Seli hizi zinapojilimbikiza huviziba vitundu vya kutolea jasho vilivyo ngozini na kusababisha chunusi sugu matakoni au kwingineko.

·         Bakteria

Bakteria ni viumbehai vidogo sana vinavyoweza kuonekana kwa kutumia hadubini tu. Viumbehai hivi ni vya aina nyingi na huweza kupatikana ardhini, hewani, na kwenye sakafu zingine. Kwa kawaida, ngozi ya binadamu huwa na bakteria nyingi sana ambazo ni muhimu sana katika kukinga ngozi dhidi ya vidubini. Lakini wakati mwingine bakteria hizi zinaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa na kuziba vitundu vya kutolea jasho na mafuta kwenye ngozi. Wingi huu wa bakteria husababishwa na uchafu na hali ya unyevunyevu kwenye ngozi yako.

Njia za Kuepuka Chunusi Matakoni

Kuna mambo ambayo unaweza kuyafanya ili kuzuia chunusi matakoni. Kwa kufuata njia hizi unapunguza pakubwa uwezekano wa kuathiriwa na ugonjwa huu wa ngozi.

1.    Dumisha Usafi

Kama tulivyotaja, chunusi zinaweza kutokea wakati seli za ngozi zilizokufa zinapokusanyika na kuziba vitundu vya kutolea mafuta na jasho ngozini. Mojawapo ya njia ya kuzuia hali hii ni kwa kuhakikisha umeoga angalau kila siku au ikiwezekana, mara mbili kwa siku.

Oga kwa kutumia maji yenye joto la kawaida au ya vuguvugu. Hii ni kwa sababu unapooga kwa kutumia maji ya moto, maji haya yanaweza yakaharibu seli za ngozi na kusababisha au kuzidisha chunusi. Kwa upande mwingine, kuoga kwa kutumia maji baridi hufanya vitundu vya ngozi vya kutolea mafuta na jasho vifungike.

Pia hakikisha kuwa unakausha mwili wote, na hasaa makalio, kwa kutumia taulo kavu kila mara. Bakteria hupenda sana kujificha katika sehemu zenye unyevunyevu. Unapokosa kukausha mwili vizuri, bakteria hizi hupata nafasi nzuri ya kuzaana na kuongezeka.

Pia hakikisha umebadilisha mavazi ya kuogelea mara tu unapotoka kwenye bwawa la kuogelea au mavazi yaliyolowa jasho baada ya mazoezi. Vaa chupi safi kila siku na ubadilishe nguo mara tu zinapochafuka. Nguo za pamba zisizobana husaidia mwili kupumua vizuri, jasho kukauka upesi, na unyevunyevu kukauka haraka hata unapotokwa na jasho.

2.    Pata Lishe Bora

Baadhi ya vyakula kama sukari, iodini, na vyakula vyenye kukaangwa na mafuta mengi husababisha ongezeko la chunusi. Kwa hivyo, ukiwa una tatizo la chunusi na vipele matakoni, ni muhimu uepeke kabisa vyakula hivi.

Pia, kumbuka kunywa maji yasiyopungua lita mbili kila siku. Maji husafisha ngozi yako na kuzuia vitundu vya ngozi kuziba.

Utambuzi na Matibabu ya Chunusi

Unapogundua kuwa makalio yako yanaonyesha mojawapo au zaidi ya dalili tulizotaja hapo awali, ni muhimu utembelee mtaalamu wa ngozi atakayekushauri kuhusu njia bora ya kutibu ugonjwa huu.

Mara nyingi, chunusi zinaweza kutambulika kwa kuziangalia na macho tu na hugawanywa katika viwango vine vikuu. Viwango hivi husaidia wahudumu kuamua matibabu yaliyo bora zaidi kwako.

Ni muhimu kujua kuwa sio vipele vyote vya mwili vinavyosababishwa na chunusi. Ikiwa hauna uhakika na visababishi vya viuvimbe matakoni, ni vyema kupata ushauri wa daktari wa ngozi.

Matibabu ya Chunusi Matakoni

Haijalishi ukali wa chunusi ulizonazo, umri wako, au aina ya chunusi uliyonayo, kuna matibabu ya kutibu chunusi za aina yoyote na katika umri wowote.

Ikiwa dalili za vipele ngozini ni hafifu tu, unaweza kuvitibu kwa kununua dawa katika duka la dawa lililokaribu nawe. Dawa mwafaka inaweza ikawa krimu, losheni, sabuni, mafuta ya kupaka, au tembe za kumeza.

Watu wanaoonyesha dalili kali za chunusi matakoni, kama vile viuvimbe vinavyowasha sana, wanapaswa watembelee daktari wa ngozi ili kupata matibabu bora na yanayofaa. Mara nyingi wagonjwa hawa hupewa tembe za kumeza zinazosaidia kukabiliana na hali hii.

Kuishi na Kukabiliana na Chunusi Matakoni

Matibabu ya chunusi makalioni yanaweza kuchukua hadi siku 28 kuonyesha mabadiliko kwenye sehemu zilizoathiriwa. Hali hii inaweza kukuathiri vibaya kihisia na kukufanya uwe na mawazo mengi au hata kushusha kujiamini kwako. Mawazo mengi yanaweza kusababisha mfadhaiko au hata ujitenge.

Ni hali ya kawaida kupatwa na hisia hizi. Lakini usiziruhusu hisia hizi zikuletee madhara zaidi. Badala yake, hakikisha unakunywa dawa zako, paka mwili wako mafuta, na usizifinye viuvimbe vile ili kuzuia alama za kudumu.

Pia kumbuka kudumisha usafi, oga kila siku, kausha mwili wako vizuri, na ubadilishe nguo zozote zilizolowa jasho au unyevunyevu wowote.   Kunywa angalau maji lita mbili kila siku na upunguze matumizi ya sukari, chumvi, na mafuta. Baada ya muda wa takriban wiki tatu hivi, utayaona matokeo na chunusi zitapona kabisa.

Ikiwa unapatwa na ugumu kukabiliana na hali hii, hasaa kama chunusi zako hujirudiarudia, ni vizuri kupata usaidizi wa mtaalamu.

Kwa maelezo zaidi tembelea ofisi zetu floor ya 8 jengo la tanzanite park.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *